WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini
kusimamia biashara ya mazao mbalimbali katika maeneo yao ili wakulima
waweze kupata tija.
Pia amesema Bodi ya Mazao
Mchanganyiko inazunguka nchi nzima kupata taarifa za bei ya mazao hayo
ili kujirisha iwapo wanunuzi wa mazao mchanganyiko ya wakulima kama
wananunua kwa bei inayostahili.
Alitoa agizo hayo jana (Alhamisi,
Julai 20, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilasilo
kilichoko katika mpaka wa mkoa wa Mbeya na Songwe alipokuwa njiani
kuelekea wilayani Songwe kwa ajili ya ziara ya kikazi.
Alisema kwa sasa bodi hiyo
inazunguna nchini kote kutafuta taarifa za bei za mazao ili kubaini bei
zinazotumiwa na wanunuzi wa mazao hayo kama zinastahili baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa wakulima wa eneo hilo.
“Wakulima msikubali kuuza mazao
ovyo, wekeni na akiba ya chakula. Pia Bodi ya Mazao Mchanganyiko
itakuja hapa kwa kuwa sasa inapita sehemu mbalimbali kupata taarifa za
bei za mazao pamoja na kuwatafutia masoko yenye tija.”
Pia Waziri Mkuu aliwaagiza watu
wote wanaohusika na suala la usambazaji wa pembejeo kuhakikisha
wanazifikisha kwa wakulima katika kipindi kisichopungua muda wa miezi
miwili kabla ya kuanza kwa msimu ili kuwaondolea changamoto ya
uchelewashwaji wa huduma hiyo
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Songwe, Bi. Chiku Gallawa alitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili
sekta ya kilimo ni kutokuwepo kwa soko la uhakika la mazao pamoja na
uingizwaji wa pembejeo zisizofaa katika mkoa.
Alisema tayari mkoa umechukua
hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuhimiza matumizi
ya teknolojia ya kisasa kama matumizi ya mbegu bora zinazostahimili
hali ya hewa iliyopo na zinazokomaa kwa muda mfupi.
Pia wataalamu wa kilimo
walichunguza pembejeo zinazotumika katika mkoa huo ambapo walibaini
asilimia 60 ya viuatilifu na asilimia 20 hadi 30 ya mbegu zinazouzwa
madukani na kutumiwa na wakulima katika wilaya za Momba na Mbozi ni
bandia.
Alisema matokeo ya kutumia
pembejeo hizo yalisababisha mavuno ya mahidi kupungua kutoka magunia 25
hadi magunia manane kwenye ekari moja katika msimu wa kilimo wa mwaka
2012/2013.
Mkuu huyo wa Mkoa alitaja
mikakati waliyojiwekea katika kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni
kufanya ukaguzi kwenye maduka yote yanayouza pembejea pamoja na kutoa
elimu ya kutambua pembejeo zisizifaa ili watoe taarifa mapema na
wahusika wachukuliwe hatua.
Post a Comment