Balozi wa mchezo wa mpira wa
kikapu nchini, Jokate Mwegelo akikabidhi bendera ya Taifa kwa mchezaji
Chipukizi, Jesca Ngaise (katikati) wakati wa hafla fupi iliyofanyika
kwenye kituo cha michezo za Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park.
Anayeshuhudia zoezi hilo ni Kocha maarufu wa mpira wa kikapu Tanzania,
Bahati Mgunda.
Balozi wa mchezo wa mpira wa
kikapu, Jokate katika picha ya pamoja na baadhi ya wachezaji chipukizi
wa mpira wa kikapu kwenye viwanja vya JMK Park.
Balozi wa mchezo wa mpira wa kikapu, Jokate akisalimiana na wachezaji chipukizi wa mpira wa kikapu kwenye viwanja vya JMK Park.
Baba Mzazji wa Jesca, Julius Ngaise akizungumza
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu
Balozi wa mchezo wa mpira wa
kikapu nchini, Jokate Mwegelo ametoa rai kwa wasichana na wazazi
kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki katika michezo mbalimbali ili kukuza
vipaji na kujiingizia kipato.
Jokate alitoa rai hiyo wakati wa
kukabidhi bendera kwa mchezaji chipukizi wa mpira wa kikapu nchini,
Jesca Julius Ngaise ambaye anaondoka leo kwenda nchini Afrika Kusini
kushiriki katika mafunzo ya juu mchezo huo yatakayoendeshwa na makocha
wa kimataifa wa ligi ya NBA ya Marekani.
Amesema kuwa Jesca ambaye ni
mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Juhudi ya Ukonga, amepata nafasi
hiyo baada ya kuchaguliwa na jopo la makocha na kuweka historia ya kuwa
msichana wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria mafunzo hayo.
“Hii ni faraja kwa Tanzania,
makocha wa kimataifa wameona kipaji cha Jesca ambaye ni nahodha wa timu
ya Taifa ya wasichana ya wachezaji wa chini ya miaka 16, ameiwezesha
Tanzania kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Afrika Mashariki
nchini Kenya, sasa tunampa bendera na kuiwakilisha nchi katika kozi
hiyo, ni sifa kubwa kwake na kwa Taifa,”
“Michezo ni ajira,wachezaji wengi
wa mpira wa kikapu wanalipwa vizuri, hii ni fursa kwa Jesca na
wachezaji wasichana, bidii inakuwezesha kufanikiwa, Jesca ni mfano wa
kuigwa na sasa anaingia katika vitabu vya kihistoria kwa kuwa msichana
wa kwanza kupata mafunzo ya NBA, akifanya vizuri anaweza kwenda
Marekani,” alisema Jokate.
Kwa upande wake, Jesca
aliwashukuru wote walioshirikiana nao katika mchezo wa mpira wa kikapu
na kuahidi kufanya vyema katika kliniki hiyo.
Alisema kuwa hakuamini kupata
nafasi hiyo na kuwaomba wasichana wenzake kujishughulisha katika michezo
kwani fursa ya kufanikiwa ipo.
“Ni faraja kwangu, wazazi wangu,
walimu na wadau wa michezo kwa ujumla, ni heshima kwa Taifa kwani
naiwakilisha nchi katika mafunzo hayo, sitawaangusha, nitafanya vizuri
na ninaamini makocha wa NBA watavutiwa na kipaji changu na kusonga
mbele,” alisema Jesca.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Mwenze Kabinda amempongeza Jesca kwa
kupata nafasi hiyo na kuomba kuongeza bidii kwani hiyo ndiyo njia ya
mafanikio.
Post a Comment