Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre
Nkurunziza leo tarehe 20 Julai, 2017 amefanya ziara ya Rasmi ya
Kiserikali ya siku moja hapa nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Ziara hiyo imefanyika katika Wilaya ya
Ngara Mkoani Kagera ambapo Mhe. Rais Nkurunziza amepokelewa rasmi kwa
kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa heshima yake katika eneo la Lemela na baadaye mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa iliyofanyika Mjini Ngara.
Baadaye viongozi hao wamezungumza na
wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Posta ya
zamani Mjini Ngara.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe.
Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemshukuru
Mhe. Rais Nkurunziza kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa
Serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano
na ushirikiano wa kihistoria na kidugu na nchi ya Burundi hususani
katika kukuza biashara na uwekezaji.
“Tanzania ni ndugu zako na
Watanzania ni ndugu wa watu wa Burundi, umekuja kwa mazungumzo ya
kiuchumi, tumezungumza mambo mengi ya kuimarisha biashara kati Tanzania
na Burundi, katika takwimu za mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na
Burundi ilikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 116.5, kiwango hiki ni
kidogo kwa nchi ya Burudni ambayo ina watu zaidi ya Milioni 10 na
Tanzania ambayo ina watu zaidi ya Milioni 52” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli
amesema Serikali ya Tanzania inaendelea na juhudi zake za kujenga reli
ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo
itaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Burundi na Rwanda na
hivyo amemhakikishia Mhe. Rais Nkurunziza kuwa reli hiyo itakuwa
kichocheo kikubwa cha uchumi wa Tanzania na nchi hizo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza
Mhe. Rais Nkurunziza kwa juhudi zake za kusimamia amani nchini mwake na
ametoa wito kwa wakimbizi wa Burundi ambao bado wapo nchini Tanzania
kuitikia wito wa Rais wao aliyewataka warudi nchini Burundi ili
wakaendelea kujenga Taifa lao kwa kuwa hali ni shwari.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kusitisha
utoaji wa uraia kwa wakimbizi hao ili utaratibu huo usitimiwe kama
kigezo cha watu kuzikimbia nchi zao.
Kwa upande wake Mhe. Rais Nkurunziza
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa mwaliko wake na amesema Tanzania na
Burundi ni ndugu na majirani ambao uhusiano na ushirikiano wake ulianza
hata kabla ya uhuru.
Mhe. Rais Nkurunziza ametoa wito kwa
wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kufanya biashara Burundi na
wafanyabisahara wa Burundi kuja Tanzania bila wasiwasi na amebainisha
kuwa hali ya Burundi ni shwari kwani hata wakimbizi waliokimbilia
Tanzania miaka miwili iliyopita wameanza kurejea nchi Burundi kwa hiari
yao na wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Tunataka kuwajulisha wenzetu
Watanzania na Warundi wenzetu ambao walikimbilia Tanzania, Burundi ya
leo ni nchi yenye amani, tunawaalika Warundi wenzetu, kaka zetu na dada
zetu ambao walikimbilia hapa Tanzania, warudi nchi kwao tujenge nchi
yetu iwe na amani ya kudumu.
Tunapata faraja kwamba Warundi
wenzetu ambao walikimbilia Tanzania miaka miwili iliyopita ambao
wanafikia idadi ya 150,000 wameanza kurudi Burundi bila ya kupitia
Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR), kwa hiyo tunasema wote rudini
nyumbani” amesema Mhe. Rais Nkurunziza.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli
ameongozana na Mawaziri watano na Mhe. Rais Nkurunziza ameongozana na
Mawaziri watano ambao pamoja na viongozi wengine wa taasisi na vyombo
vya ulinzi na usalama wameshiriki mazungumzo rasmi.
Mhe. Rais Nkurunziza amemaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku moja hapa nchini na amerejea nchini Burundi.
Kesho tarehe 21 Julai, 2017 Mhe. Rais
Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kigoma ambapo ataweka jiwa la
msingi la ujenzi wa barabara ya Nyakanazi – Kibondo na barabara ya
Kidahwe – Kasulu pamoja na kuzungumza na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Ngara, Kagera
20 Julai, 2017
Post a Comment