Idara ya Uhamiaji imesema
jukumu la Udhibiti wa Uingiaji na Utokaji wa raia wa kigeni nchini,
linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 (Rejeo la
2016) na wala haiwalengi wafanyakazi wa Kampuni ya Madini ya Acacia
peke yake.
Ni hitajio la kisheria kwa kila
raia wa kigeni anayeingia na kutoka nchini kukaguliwa ili
kujiridhisha iwapo hakuna dosari zozote za Uhamiaji, Ulinzi na
Usalama.
Sheria ya Uhamiaji inaitaka Idara
ya Uhamiaji kumhoji mtu yeyote awe raia wa Tanzania au kigeni bila
kujali anafanya kazi kwenye Kampuni au Shirika gani, pale inapotaka
kujiridhisha juu ya uhalali wa ukaazi wake hapa nchini na
ikijiridhisha kuwa mtu huyu hana dosari zozote inamwachia huru kama
ilivyofanyika kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Madini ya Acacia
waliohojiwa na kuruhusiwa kuendelea na safari yao hivi karibuni.
Idara ya Uhamiaji inapenda
kuuarifu Umma kuwa hakuna sababu zozote nje ya matakwa ya Sheria ya
Uhamiaji zinazopelekea Idara ya Uhamiaji kuweka kizuizi cha kuja au
kutoka kwa wafanyakazi wa kigeni wa Acacia.
Tunapenda kuujulisha Umma kuwa
ni muhimu kwa watanzania na raia wa kigeni wanaokusudia kuingia na
kutoka nchini kuhakikisha wanafuata Sheria za Uhamiaji ili kutimiza
hitajio la kisheria.
Imetolewa na
Ally M. Mtanda
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji
29 Julai 2017
Post a Comment