WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao.
Amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Julai 19, 2017 wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe Bibi Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela.
Amesema Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.
"Tutashughulika na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka walizonazo."
Pia amewaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake na kwamba Serikali inawategemea na iko pamoja nao.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya Askofu wa Kanisa la Evarinjerical Brother Hood, Rabison Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu kumtukana Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli.
Amesema ni vema watu hao wakajifunza namna ya kuwasilisha hoja zao bila ya kutumia lugha za matusi.
“Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya maendeleo. Wanaofanya hivyo wasidhani kama wanamtukana Rais tu bali wanawatukana Watanzania wote waliomchagua wakiwemo viongozi wa dini.”
Pia aliwaomba wananchi kufanya maandalizi mapema kwa sababu wote ni wapitaji, hivyo waandae roho zao kwa kuacha kufanya dhambi na maovu yote ili wawe na mwisho mwema.
Vile Vile Waziri Mkuu amewaomba wananchi wote washirikiane kwa pamoja kumuombea Dkt. Mwakyembe na familia yake ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.
“Wajibu wetu sote ni kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema. Tunajua kwa sasa Dkt. Mwakyembe yuko katika wakati mgumu, namuhakikishia kwamba hayuko peke yake kwani Serikali iko pamoja naye katika kipindi hiki kigumu.”
Naye, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai alimpa pole Dkt. Mwakyembe huku akiitaka familia kuendelea kuwa na upendo kama ule uliokuwepo wakati wa uhai wa marehemu Bibi Linnah.
Kwa upande wake, Mtoto mkubwa wa marehemu, George Mwakyembe alisema anaamini mama yao, alijiandaa na kifo hicho kwa kuwa alikuwa mchamungu.
"Mama alikuwa na ratiba kila siku ifikapo saa nne usiku lazima afanye ibada, Hivyo nina matumaini makubwa kupitia Uchamungu wake, Mwenyezi Mungu atamuweka mahala pema."
Post a Comment