WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametembelea na kufanya ukaguzi katika eneo la mradi wa ujenzi wa gati
kwenye Manispaa ya Lindi na kusema kwamba ameridhishwa na utekelezaji
wake.
Pia amewaagiza viongozi wa Wakala
wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Lindi kujenga eneo la kupumzikia
abiria kwenye maegesho ya kivuko katika maeneo ya Lindi na Kitunda ili
wananchi wa maeneo ya Lindi na Kitunda waanze kupata huduma ya kivuko.
Waziri Mkuu alitembelea mradi huo
jana (Ijumaa, Julai 14, 2017) wakati alipotembelea eneo hilo kwa lengo
la kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati hilo, akiwa katika ziara yake ya
kikazi mkoani Lindi.
Alisisitiza kuwa Serikali ya
awamu ya tano imedhamiria kuondoa kero ya usafiri kwa wakazi wa maeneo
hayo, hivyo ujenzi wa gati hilo uende kwa kasi huku ukizingatia matakwa
ya kiufundi na ubora wa hali ya juu.
“Jengeni sehemu ya kupumzikia
abiria katika pande zote mbili, upande wa Lindi na wa Kitunda. Mbali na
abiria kupata eneo la kupumzikia pia itarahisisha hata ukataji wa tiketi
jambo litakawarahisishia ukusanyaji wa mapato.”
Pia Waziri Mkuu aliwaomba
wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana na Serikali katika shughuli
mbalimbali za maendeleo na kwamba ahadi zote zilizoahidiwa katika Ilani
ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zitatekelezwa.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi kuyafanyia maboresho
maeneo ya pwani na kuwa ya kisasa kwa kuondoa majengo yote chakavu ili
wananchi waweze kuyatumia kwa ajili ya kupumzikia.
Alisema ni vema kwa manispaa hiyo
kuainisha majengo yote ya zamani yaliyoko katika upande wa pwani
yanayotakiwa kuhifadhiwa kwa ajili ya makumbusho ili yaweze kukarabatiwa
na yaliyosalia yaondolewe.
Pia Waziri Mkuu alitembelea chuo
cha Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Lindi na kusema kwamba
ameridhishwa na utoaji wa elimu chuoni hapo na kuwaagiza viongozi
waanzishe mafunzo ya mafuta na gesi ili vijana waweze kupata ujuzi na
kuajiriwa kwenye sekta hiyo.
Post a Comment