WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu
ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha kwamba programu zote zinazotolewa na
taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kujiajiri na kuwa na sifa
za ushindani katika soko la ajira kimataifa.
Amesema wakati umefika sasa kwa
wasomi katika vyuo vyetu vikuu tujiridhisha kuwa mitaala inayotolewa
kama inawaandaa wahitimu kupata taaluma na stadi za kuweza kujiajiri na
kupambana na changamoto za kimaisha.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 26, 2017) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 12 ya Elimu ya Juu, jijini Dar es Salaam.
Amesema taasisi za elimu ya juu
nchini ziangalie mitaala yake na kuimarisha mfumo wa ithibati na
udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ili kwenda sambamba na dunia ya
kazi inayoendana na agenda ya maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu amesema maonesho hayo
ni jukwaa la kipekee ambalo litaibua mjadala sahihi kuhusu uhalali wa
kozi zinazotolewa na vyuo husika vya elimu ya juu. “Hivyo mnayo nafasi
ya kuonesha kwa vitendo uwezo wenu katika utafiti, ubunifu na matumizi
ya sayansi na teknolojia zinazotumika katika maendeleo ya viwanda.”
Amesema ni vema mfumo wa ithibati
na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ukaimarishwa ili kuhakikisha
asilimia 60 ya wanafunzi wanahitimu shahada kwenye sekta ambazo
zinachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi.
Amesema taasisi za elimu ya juu
ziweke mikakati ya kuinua na kuboresha taaluma wanayoitoa ili ilete
tija kwa maendeleo ya Taifa na Dunia. Pia kuanzisha program za mafunzo
zenye kukidhi mahitaji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa
kuzingatia mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amezitaka
taasisi hizo kuendelea kuimarisha mfumo wa udahili na kujipanga kutumia
fursa za elimu na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi yote ya jamii
kwa usawa katika ngazi zote hususan ufundi, hisabati, sayansi na
teknolojia.
Pia Waziri Mkuu amesema ni wakati
muafaka kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuandaa mikakati ya kuongeza
udahili kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali watu na ujuzi unaohitajika
katika sketa zinazokua haraka mfano mafuta, gesi na madini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, JULAI 26, 2017
Post a Comment