Naibu Waziri Ofisi ya Rais
Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na wakurungenzi wa Halmashauri na
Wakuu wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa wakati wa kufunga mafunzo ,ikiwa
ni mwendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa
Serikali yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Baadhi ya Wakurungenzi wa
Halmashauri za Mikoa sita ya kanda ya ziwa wakishiriki mafunzo ya
kuwajengea uwezo viongozi yaliyotolewa na Taasisi ya Uongozi kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.
…………………………………………………………………………………….
Serikali imewaagiza Wakuu wa
wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri nchini kwenda kusimamia mipango ya
maendeleo baada ya kupitishwa kwa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha
2017/2018.
Hayo yalisemwa leo na Naibu
waziri wa nchi, Ofisi ya Rais. Tamisemi Selemani Jafo kwa niaba ya
Waziri mkuu Kassim Majaliwa katika kufunga semina ya siku tano kwa wakuu
wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri mjini Dodoma.
Semina hiyo ya uongozi imelenga
kuwajengea uwezo viongozi hao ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo
na imetolewa na wataalam wa Taasisi ya Uongozi ikishirikiana na ofisi ya
Rais Tamisemi.
Mafunzo hayo ni ya awamu ya pili
na yamejumuisha viongozi hao kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Manyara,
Kagera, Simiyu na Shinyanga huku awamu ya kwanza yalihusisha mikoa ya
Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Katavi na Kigoma.
Akifunga mafunzo hayo, Jafo
amesema inatarajiwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote
watapata mafuzo hayo kwa awamu kabla ya mwezi Septemba mwaka huu.
Amewataka kuweka mipango kazi kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
Jafo amesema katika kusimamia
mipango hiyo wahakikishe wanatoa kipaumbele katika kusimamia sekta
muhimu ambazo zinagusa jamii kama Afya, Elimu na Maji.
“Jiepusheni na uzalishaji wa
madeni,hakikisheni malipo hewa, safari hewa, watumishi hewa hawatokei
katika maeneo yenu mnayosimamia,”amesema Jafo
Aidha, Jafo amewatahadhari
kujiepusha na watu wanaofanya vitendo vya utapeli kwa kutumia majina na
picha za viongozi wa juu ikiwemo Mawaziri ili kujipatia fedha.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi
wa Taasisi ya Uongozi,Denis Rweyemamu,amesema mafunzo yanalenga
kuwajengea uwezo ili waweze kufanya kazi kwa weledi.
Post a Comment