Waziri wa Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiongea na
waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Katibu Mkuu
kutoka Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel na kulia ni Mwenyekiti wa
Kampuni ya Star Times Bw. Xinxing Pang.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe
(hayupo katika picha) alipokuwa akieleza msimamo wa Serikali kuhusiana
na Kampuni ya Star Times jana Jijini Dar es Salaam. (Picha na Lorietha
Laurence.)
…………………………………………………………………………
Na Lorietha Laurence -WHSUM.
Waziri wa Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameunda kamati ya wajumbe
10 kwa ajili ya kufuatilia undani wa kutopatikana kwa faida kati ya
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kampuni ya Star Times kutoka
China.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana jijini Dar es Salaam alisema kuwa kamati hiyo imepewa siku
saba kuhakikisha inakuja na taarifa kamili kuhusiana na suala hilo.
“ nimeipa kamati hii muda wa
siku saba ukimalizika siiongezi tena nitatoa labda siku moja mbili
kumalizia tu ili inipatie majibu kamili kwa nini kwa miaka yote hiyo
hakuna faida”alisema Mwakyembe.
Aidha Dkt. Mwakyemba anaeleza
kuwa uamuzi wa kuunda kamati hiyo ni kutokana na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kuonyesha kukerwa na kutokupatikana kwa faida kwenye
ushirikiano huo wa TBC na Star Times alipofanya ziara yake mwezi Mei
mwaka huu.
Anazidi kufafanua kuwa Rais
alikasirishwa na kitendo cha kampuni hiyo kufanya kazi nchini kwa
kipindi cha miaka saba bila faida yoyote na hivyo kuagiza hatua
stahiki kuchukuliwa juu ya suala hilo.
Dkt. Mwakyembe anabainisha kuwa
tangu kutolewa kwa kauli ya Rais Mhe. Dkt. Magufuli Wizara na watendaji
wake tayari wameshafanya mikutano miwili mmoja Mjini Dodoma na mwingine
Jijini Dar es Salaam wakajadili kwa kina sababu zinazopelekea kushindwa
kupatikana kwa faida.
Kabla ya mkutano na waandishi wa
habari ,Waziri Dkt. Mwakyembe alitumia takribani saa tatu akijadiliana
kwa kina na Mwenyekiti wa Kampuni ya Star Times kutokea nchini China,
Xinxing Pang pamoja na wafanyakazi wa wizara akiwamo Katibu Mkuu Profesa
Elisante Ole Gabriel na Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt.Hassan
Abbas.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Star Times Bw. Xinxing Pang alisema kuwa ana imani kuna uwezekano wa
kumalizwa kwa suala hilo kwa kutumia wataalamu wake watakaoangalia
sababu za kutokupatikana kwa faida na nini kifanyike katika kuondokana
na changamoto hiyo.
Post a Comment