WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema kuanzia mwaka huu wa fedha, Serikali imepunguza gharama za
malipo ya awali ya thamani ya ardhi iliyopimwa kutoka asilimia 7.5 hadi
asilimia 2.5.
“Serikali inaendelea kupunguza
gharama za umilikaji wa ardhi nchini na katika mwaka wa fedha
2017/2018, imepunguza tozo ya awali ya ardhi iliyopimwa (premium) kutoka
asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu. Natoa wito kwa
wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na
kumilikishwa ardhi,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja
ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi
Septemba 5, mwaka huu.
Amesema Serikali itahakikisha
kuwa kila kipande cha ardhi ya Tanzania kinapimwa ikiwa ni utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. “Serikali imeweka mkakati na
mpango kazi wa kuwezesha kufikia lengo la kupanga matumizi bora ya ardhi
katika vijiji 1,500 na wilaya tano kila mwaka.”
Amesema Serikali itaendelea
kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda kwa kupeleka wataalam wa kada
mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi stahiki. “Kazi ya
upimaji wa ardhi haiwezi kufanikiwa bila ya rasilmali watu. Lengo letu
ni kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za ardhi katika kanda
badala ya kufuata huduma hizo makao makuu ya wizara,” amesema.
Amewasihi watumishi
watakaohamishiwa katika ofisi za kanda pamoja na wale waliopo katika
Halmashauri, wafanye kazi kwa ushirikiano na watekeleze majukumu yao kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya ardhi na
kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
40480 – DODOMA.
JUMATANO, JULAI 5, 2017.
Post a Comment