Na Daudi Manongi-DODOMA.
Serikali kupitia Wizara ya
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo inaendelea na mchakato wa kuanzisha
Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa ili kusaidia kuinua kipato,kuongeza tija na
kukuza uwezo na weledi kwa Wasanii nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi, Anastazia Wambura wakati akijibu
hoja mbalimbali za wabunge Mjini Dodoma.
“Serikali inategemea kuweka
utaratibu mzuri wa upatikanaji fedha na hivyo kuwawezesha Wasanii
kuzalisha kazi bora za Sanaa zenye kukidhi viwango vya masoko ya ndani
na nje ya nchi”, Alisema Mhe.Wambura.
Aidha amesema katika kipindi hiki
ambacho Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa unaandaliwa Serikali inashauri
Halmshauri zote ziwasaidie vijana wanaojishughulisha na Sanaa kwa kuwapa
mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa ajili ya mitaji kutoka kwenye
asilimia 10 ya mapato ya kila Halmashauri kwa kuwa Sanaa pia ni sehemu
ya ujasiriamali na ni chanzo kikubwa cha ajira kwa Vijana nchini kwa
sasa.
Akizungumzia suala la haki miliki
amesema kupitia Bodi ya Filamu,COSOTA na BASATA zimeendelea kuwaelimisha
wasanii wa fani mbalimbali kusajili kazi zao ili ziweze kutambuliwa
,kupata udhibiti na ulinzi kutokana na wizi wa kazi za sanaa.Aidha
Serikali inaendelea kushughulikia migogoro na biashara haramu ya
kudurufu kazi za sanaa ili wasanii waweze kuongeza kipato chao.
“Haki na maslahi ya wasanii
yanalindwa kwa Sheria Na.7 ya mwaka 1999 ya Hakimiliki na
Hakishiriki,Sheria Na.4 ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya 1976 na
Sheria Na.23 ya Baraza la Sanaa la Taifa ya 1984 na Serikali inaendelea
na mabadiliko ya Sheria hizi ziendani na wakati Alisema”, Mhe.Wambura.
Serikali inaendelea na
Urasimishaji wa Tasnia ya Filamu na Muziki ambapo kazi za wasanii hawa
zinawekewa stempu za TRA ambazo huwezesha kubaini nakala halisi.
Post a Comment