Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali imeahidi kuwa
italirejeshea Shirika la Posta Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 3.2
ambazo ilizitumia kuwalipa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na
Simu la Afrika Mashariki ifikapo kufikia 30 Juni mwaka huu itakuwa
imelipa kiasi cha Sh. Bil.3.2 zinazodaiwa na Shirika la Posta Tanzania
Ahadi hiyo imetole Bungeni Mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na MIpango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,
alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ludewa, Mhe. Deo
Ngalawa (CCM), aliyehoji Serikali ilikuwa na mpango gani wa kuwalipa
Wastaafu hao yenyewe moja kwa moja bila ya kutumia fedha za mfuko wa
Shirika hilo.
‘’Shirika linasuasua kujiendesha,
fedha ambazo zilikuwa zitumike kwenye operation ndizo hizo zimekuwa
zikitumika kuwalipa Wastaafu wa Afrika Mashariki ili kulinusuru Shirika
hilo serikali haioni umuhimu wa kulipa deni hilo”.alihoji Mhe. Ngalawa.
Mhe, Ngalawa alitaka kujua kwanini
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mwaka 2016 ilifungia akaunti za
Shirika la Posta Nchini, kutokana na kuliidai Shirika hilo kiasi cha
Sh. Mil.600, ikiwa Shirika hilo linaidai Serikali kiasi cha Sh. Bil.5.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji
alisema kuwa, Serikali ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha fedha hizo
zinalipwa na Serikali yenyewe na sio Shirika.
Aliongeza kuwa watumishi wote wa
Shirika hilo wamekwisha jiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii, na
wanachangia katika mifuko mbalimbali hivyo wakistaafu mifuko hiyo
itakuwa ikiwalipa mafao yao na si Serikali tena.
Naibu waziri huyo aliongeza kuwa
Serikali itaendelea kulipa madeni hayo kadri fedha zitakapopatikana,
watahakikisha ifikapo Juni 30 mwaka huu fedha zote zinazodaiwa na
Shirika hilo zitakuwa zimelipwa.
Katika swali la msingi, Mhe.
Ngalawa , alitaka kujua mpango wa Serikali wa kulirejeshea Shirika fedha
ambazo lilitumia kuwalipa Wastaafu waliokuwa Shirika la Posta na simu
la Afrika Mashariki, kunusuru Shirika hilo.
Akijibu hoja hiyo Dkt. Kijaji
alikiri kuwa Shirika limekuwa likitumia fedha zake kuwalipa Wastaafu wa
lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki na kuwasilisha
madai Serikalini ili lipate kurejeshewa fedha zake.
Aliongeza kuwa hadi sasa Shirika
limelipa Sh. Bil. 5.9 na Serikali imesharejesha kiasi cha Sh. Bil. 2.7,
alisema malipo hayo yamekuwa yakilipwa kwa awamu ambapo kwa mwezi
Novemba 2016 kiasi cha Sh. 700,000,000, Desemba 2016 Sh. 1,000,000,000
na Januari 2017 Sh. 1,000,000,000.
Dkt. Kijaji amesema pia kuwa
Serikali itaendelea kurejesha kiasi kilichobaki cha Sh. 3,200,000,000
kadri fedha zitakavyopatikana.
‘Serikali kupitia Msajili wa
Hazina inaendelea na jukumu la kuwalipa Pensheni ya kila mwezi Wastaafu
wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki wapatao 292’.
Aliongeza Dkt. Kijaji.
Post a Comment