Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Samia
Suluhu Hassan akizungumza na wajumbe wa Kamati tekelezaji za UWT ngazi
za Wilaya, Mikoa na Taifa Unguja, huko Afisi Kuu Kisiwandui.
…………
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.
JUMUIYA ya Wanawake wa CCM (UWT)
wametakiwa kutumia uwezo, weledi, nguvu na ushawishi waliokuwa nao
kisiasa kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinafanikisha kwa ufanisi
Uchaguzi wa ndani ya Chama ili ipatikane timu imara ya viongozi
watakaofanikisha Ushindi wa Dola katika Uchaguzi Mkuu 2020.
Nasaha hizo zimetolewa na Mjumbe
wa Kamati Kuu wa CCM, Mh. Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na
Wajumbe wa Kamati Tekelezaji wa ngazi za Wilaya, Mikoa hadi Taifa wa
UWT, huko Afisi Kuu CCM Kisiwandui Zanzibar alipohitimisha ziara yake ya
kuimarisha Chama hicho nchini.
Alifafanua kwamba UWT wanatakiwa
kwa mstari wa mbele kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi huo inafanyika
kwa ufanisi kwa lengo la kupata jopo la viongozi na watendaji waadilifu
na wenye uwezo wa kusoma alama za nyakati kisiasa na kijamii.
Pia aliendelea kueleza kwamba
wanawake wa Umoja huo ni miongoni mwa rasilimali watu wanaotakiwa
kukitumikia chama kwa bidii ili kiweze kufikia malengo yake ya
kuendeleza ushindi wa Dola kwa kila uchaguzi mkuu wa kisiasa.
Mh. Ambaye pia ni Makamo wa Pili
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwambia Akina Mama hao
kwamba mikakati hiyo itafanyika kwa ufanisi endapo kila mtu ndani ya
umoja huo atakuwa tayari kutumia kipaji chake cha kisiasa kuhakikisha
analinda na kutetea maslahi ya chama kwa vitendo.
“ Wanawake tutumieni uwezo wetu
katika kujenga ushawishi na hamasa kwa kuongeza wanachama wapya
watakaokubali kuwa na itikadi ya kweli ya CCM.
Pamoja na mipango yetu ya
kuimarisha chama tusisahau kuzidisha umoja na upendo miongoni mwetu kwa
kuacha baadhi ya mambo yasiyofaa na tunayohisi hayana maslahi na Chama
pamoja na jumuiya yetu”, alisema Mh.Samia na kuongeza kuwa lazima
viongozi waliopewa dhamana ndani ya umoja huo wafanye kazi kwa bidii
ili wananchi waendelee kujivunia uwepo wa Chama hicho katika medali za
kisisasa Visiwani Zanzibar.
Pamoja na hayo alisisitiza umuhimu
wa wanachama wa chama hicho hasa Wazee kuwarithisha watoto wao
miongozo na itikadi za ASP ambayo ni CCM, ili waweze kukua wakiwa
katika misingi ya weledi na ukada wa kweli ambazo ni nyenzo
zitakazowasaidia pindi watakapokuwa viongozi wa chama na serikali wa
baadae.
Hata hivyo aliwataka viongozi na
watendaji kuhakikisha takwimu za wanachama wanazoratibu zinakuwa sahihi
ili ziweze kusaidia katika tathimini mbali mbali za kisiasa nchini hasa
kabla na baada ya uchaguzi.
Akitoa ufafanuzi juu ya Uchaguzi
wa chama unaoendelea kwa hatua ya uchukuaji wa fomu kwa ngazi ya Matawi
na mashina, Katibu wa NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Bi.
Waride Bakar Jabu amesema nafasi zinazochukuliwa fomu kwa mtu mmoja ni
zile za kiutendaji ambazo ni Katibu na Mwenyekiti lakini nafasi zingine
zote zilizobaki zinatakiwa kuchukuliwa fomu zaidi ya mtu mmoja.
Akizungumza katika kikao hicho,
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar , Bi. Tunu Juma Kondo alisema
umoja huo umekuwa ukishiriki ipasavyo katika majukumu mbali mbali ya
chama na kuhakikisha yanafanyikana na kukamilika kwa wakati.
Aidha aliahidi kwamba umoja huo
utafanya kila linalowezekana kuhakikisha Uchaguzi ndani ya taasisi hiyo
unafanyika vizuri kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya Katiba ya CCM ya
mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake.
Naye Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Bi. Maudline Cyrus Castico,
akitoa ufafanuzi juu ya kesi za udhalilishaji wa kijinzia nchini,
alisema kwa sasa wanaendelea na kutoa elimu kwa jamii juu ya kuwa na
muamuko wa kutoa ushahidi mahakamani huku wakiandaa mikakati imara ya
kusimamia vyombo vya kisheria vitende haki kwa watu wanaofanya uhalifu
huo.
Kwa upande wao viongozi mbali
mbali wa umoja huo kutoka Mikoa ya Zanzibar kichama walipewa fursa ya
kutoa maoni na ushauri wao, ambao walipendekeza kwamba CCM kupitia idara
husika ziendeleze madarasa ya Itikadi kwa vijana mbali mbali ili kupata
viongozi wa baadae walioiva kisiasa.
Akizungumza miongoni mwa waasisi
wa ASP, Bi.Asha Simba aliwataka vijana wa Chama hicho kuvaa joho la
Vijana wa enzi za ASP waliokomboa Zanzibar kutoka katika mikono ya
utawala wa kimabavu, na wao wafuate nyayo hizo kuendeleza heshima ya CCM
kwa sasa.
Post a Comment