Na Nuru Juma & Husna Saidi- MAELEZO
Waandishi wa Habari nchini
wametakiwa kuzingatia kanuni,sheria na taratibu za uandishi katika
kuandika habari zitakazoleta umoja,mshikamano na maendeleo na siyo
uchochezi ili kujenga jamii bora.
Hayo yamesemwa leo Jijini Mwanza
na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Harrison George
Mwakyembe kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya
Habari Duniani.
Dkt. Mwakyembe aliongeza kwa
kusema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa siku ya uhuru wa vyombo vya
habari ambapo siku hiyo huwa maalum kwa wadau wa tasnia hiyo kukutana na
kujadiliana mambo mbalimbali ikiwa ni njia ya kujenga jukwaa la
ushirikiano.
“Uhuru wa habari una ukomo wake
hivyo ni muhimu kwa vyombo vya habari hapa nchini kuajiri watu wenye
taaluma hiyo kwa kuachana na makanjanja ili viheshimike kwa kutoa
taarifa zenye kuzingatia maadili ya uandishi”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Alizidi kufafanua kuwa katika
kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, kalamu ya
mwandishi wa habari itetee ukweli na si mambo ya haramu kwa sababu ya
siasa au rushwa ambayo huwa kichocheo cha uvunjifu wa amani.
Aidha aliitaka Idara ya Habari
(MAELEZO) kuwa na utaratibu wa kukutana na wahariri kila mwezi ili
kuweza kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia nzima ya
habari nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi alisema uandishi wa habari
si biashara ya kawaida bali ni kazi yenye kuhitaji uweledi mkubwa hivyo
waandishi wanatakiwa kufuata taratibu na sheria za uandishi
Post a Comment