Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya Mkutano wa Tano wa Sayansi ya Afya waChuo Kikuu cha Afya
na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) Dk. Irene Kida akitoa
majumuisho ya Mkutano huo mbele ya Mkurugenzi wa Elimu ya juu, Wizara ya
Elimu, Sayansi, teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temu
(wa tatu kushoto meza kuu) wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha mkutano
huo uliofanyika kwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Wengine ni
pamoja na walimu na uongozi wa chuo hicho akiwemo Kaimu Naibu Makamu
Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa ( wa pili kushoto)
Mkurugenzi wa Elimu ya juu, Wizara
ya Elimu, Sayansi, teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temu
(wa pili kushoto) akisikiliza maelezo kuhusiana na dawa za asili
zinazoandaliwa na kitengo cha tiba asili katika Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) alipotembelea maonyesho ya
shughuli zinazofanywa na MUHAS mara baada ya kuhitimisha Mkutano wa tano
wa kisayansi ulioandaliwa na chuo hicho jijini Dar es Salaam mwishoni
mwa wiki iliyopita. Wanaoshuhudia ni pamoja na viongozi wa Chuo hicho
akiwemo na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa
(kushoto)
…………………………
Na Mwandishi wetu,
SERIKALI imetoa wito kwa taasisi
za elimu ya afya na mashirika mbalimbali yanayofanya tafiti za afya hapa
nchini kuhakikisha tafiti hizo zinafika kwa wadau na wananchi kwa
ujumla ili zilete tija zaidi kwa jamii badala ya kuzifungia kwenye ofisi
zao.
Wito huo wa serikali ulitolewa
mwisho wa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Elimu ya juu,
Wizara ya Elimu, Sayansi, teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa
Sylvia Temu alipomuwakilisha Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk. Leonard
Akwilapo kwenye hafla ya kuhitimisha Mkutano wa tano wa kisayansi
ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili
(MUHAS).
“Kwa sasa tunaelekea kwenye uchumi
wa viwanda na miongoni mwa sekta muhimu ambazo pia zinatarajia
wawekezaji ni pamoja na sekta ya afya hivyo basi muelekeo na mapendekezo
ya tafiti za afya ndio zitakazoweza kuwasaidia wadau na serikali
kufahamu aina ya ukwekezaji huo pamoja na maeneo gani yanafaa kulingana
na mahitaji. Tafiti hizi zikifungiwa kwenye makabati tafsiri yake ni
kwamba hata hii mikutano itakosa tija pia.’’ alisisitiza.
Aliongeza kuwa Serikali kwa kiasi
kikubwa inajitahidi kutumia tafiti hizo katika kuandaa sera mbalimbali
zinazohusiana na masuala ya afya huku akitoa pongezi kwa uongozi wa chuo
hicho kwa kuendelea kuandaa wataalamu wanaoandaa tafiti hizo kwa weledi
na ufanisi mkubwa.
“Zaidi umuhimu wa mkutano huu ni
pale unapowakutanisha wataalamu wa afya tena katika ngazi tofauti
wakiwemo wale waliobobea pamoja na wanafunzi na hivyo kuwa kama jukwaa
kwa wao kuweza kubadilishana ujuzi. Jumla ya tafiti 160 tofauti za afya
zimewasilishwa kupitia mkutano huu ambapo tafiti 70 kati ya hizo
zilijadiliwa kwa kina na wataalamu hawa,’’ aliongeza.
Awali, akizungumza kwenye hafla
hiyo Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa
alisema nyingi kati ya tafiti zilizowasilishwa kwenye mkutano huo wa
siku mbili zilijikita katika vipaumbele vya taifa yakiwemo masuala ya
HIV/AIDS, kifua kikuu, afya ya uzazi na mtoto, magonjwa yasiyo ya
kuambukiza, ajali pamoja na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika.
“Ndio maana tunaishukuru sana
serikali ya Sweden kupitia Shirika la Sida ambao kwa kushirikiana na
wadau wengine wamewezesha mkutano huu muhimu.,’’ alisema Prof Kamuhabwa
huku akibainisha kuwa chuo hicho kimejipanga kuhakikisha tafiti hizo
zinawafikia walengwa ikiwemo Serikali, mashirika na taasisi mbalimbali
pamoja na wananchi kwa ujumla.
Post a Comment