Mnamo tarehe 18 Machi 2017 Ujumbe
wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dk. Cleopa Mailu
uliwasili nchini ambapo ulikutana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya
kuomba kuajiri kwa Mkataba Madaktari wa Tanzania mia tano (500) ili
kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya. Mheshimiwa Rais alikubali
ombi hilo.
Tarehe 18 Machi, 2017 Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitangaza nafasi hizo
za ajira kwa Madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya.
Maombi hayo yalipokelewa ambapo hadi tarehe 27 Machi, 2017 ambapo jumla
ya maombi takribani 496 yaliwasilishwa. Baada ya kufanya uchambuzi wa
maombi haya ilibainika kuwa, Madaktari 258 walikidhi vigezo
vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Baadhi ya vigezo hivyo
ni pamoja na:
- Uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya Sekondari.
- Chuo alichosoma na mwaka wa kuhitimu masomo.
- Sehemu alikofanya mafunzo ya vitendo (Intership) na mwaka wa kuhitimu mafunzo hayo.
- Uzoefu wa kazi.
- Umri wa mwombaji usizidi miaka 55.
- Usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari la Tanganyika.
- Asiwe mtumishi wa Umma, Hospitali Teule za Halmashauri na Hospitali za Mashirika ya hiyari wanaolipwa mishahara na Serikali.
Wakati Serikali ya Tanzania
ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari wake nchini Kenya
ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi hizo za kazi na kufanya uchambuzi
wa maombi ya kazi, kuandaa Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya
Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo za Madaktari na Mkataba
wa Ajira kwa Madaktari hao, wananchi (Madaktari) watano wa Kenya
waliwasilisha pingamizi Mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao
kusitisha kuajiri Madaktari kutoka Tanzania.
Kwa kuwa ratiba ya utekelezaji wa
ajira hizi za Madaktari ilikubalika na pande zote mbili kuwa iwe
imekamilika ifikapo tarehe 6 Aprili, 2017 na kuwa Madaktari hao wawe
tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili, 2017 na
kwa kuwa hadi tarehe ya taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa
pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za Madaktari wa Tanzania nchini
Kenya, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ameamua kuwa, Madaktari hao 258 ambao waliokuwa tayari
kwenda kufanya kazi nchini Kenya waajiriwe na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mara moja. Kufuatia uamuzi huu, Majina ya Madaktari
husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya
Wizara www.ehealth.go.tz pamoja na wataalamu wengine wa Afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.
Aidha, Serikali ya Tanzania
itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa
Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kupeleka Madaktari
wetu nchini Kenya.
Imetolewa na:
Ummy A. Mwalimu (Mb),
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto,
Chuo Kikuu cha DODOMA,
S.L.P. 743,
DODOMA.
19 Aprili, 2017
Post a Comment