Na Zawadi Msalla-WHUSM
Viongozi wa kimila Mkoani Mbeya waunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika hatua mbalimbali za kuhakikisha Tanzania inafika katika uchumi wa kati wa Viwanda .
Wameyasema hayo walipokuwa wakizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel katika ziara yake Mkoani humo na kuongeza kuwa ni vema Watanzania waungane kwa pamoja kufanikisha nia njema ya Rais, Dkt. Magufuli.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi hao ,Chifu Rocket Mwashinga kutoka Igawilo alisema kuwa Rais anasisitiza wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuondokana na umaskini na kulijenga taifa.
“Tufikishie ujumbe huu kwa Mhe. Rais ili hao vijana wetu wanaokimbilia mijini badala ya kukaa na sisi wazee kulima nchi isiwe na njaa warudishwe vijijini waje walime na kwa maendeleo yao binafsi na taifa”
“Inasikitisha sana kuona siku hizi vijana wakilalamikia Serikali kuwa maisha ni magumu wakati wameacha mashamba na wao ndiyo watu wenye nguvu ambapo magenge makubwa ya ujambazi, wabakaji na walevi waliopitiliza yaliyopo huko mijini yanatokana na vijana wasio na ajira” Alisema Chifu Mwashinga.
Aidha Wakuu hao wa kimila walieleza kuwa ili kauli mbiu ya Hapa Kazi tu iweze kutekelezeka wameiomba Serikali iangalie utaratibu wa kuwarudisha vijijini vijana wasio na ajira waliopo mijini kwa kuwa wao ndio nguvu kazi na chachu ya maendeleo.
Pia viongozi hao waliishauri Serikali kufufua kilimo shuleni ambapo hapo awali watoto walifundishwa elimu ya kujitegemea kwa kulima mashamba na kujenga majengo ya shuleni mambo ambayo kwa sasa hayafanyiki.
“Tulifundishwa kupenda kilimo tukiwa shuleni ,watoto wa siku hizi hata jembe hawajui kulishika” Alieleza Chifu Joseph Mwalawa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel aliiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuwatambua wakuu hao wa kimila ili kwa pamoja waweze kusukuma gurudumu la Maendeleo ya taifa.
Post a Comment