Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara
Nchini (TANROADS), mkoa wa Singida, Eng. Yohanes Mbegalo, akitoa
taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani (Wa kwanza kulia), kuhusu maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi wa
Daraja la Sibiti lenye urefu wa M 82 linalounganisha Mikoa ya Singida,
Simiyu, Manyara na Mara.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri
Mr. Sunil Singh( Wa tatu kulia), anayesimamia mradi wa ujenzi wa Daraja
la Sibiti lenye urefu wa M 82 na barabara za maingilio kwa kiwango cha
changarawe KM 25, mkoani Singida jana.
Mhandisi Mshauri Mr. Sunil Singh,
akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani (kulia), nguzo za Daraja la Sibiti zilizosimamishwa wakati
alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja hilo na barabara za maingilio kwa
kiwango cha changarawe KM 25, mkoani Singida jana.
Muonekano wa nguzo za Daraja la
Sibiti lenye urefu wa Mita 82 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 48.
Daraja hilo ni kiungo muhimu kwani litaunganisha Wilaya ya Iramba na
Mkalama mkoani Singida na Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Mwananchi Petro Daudi, kutoka
Wilaya ya Meatu akimweleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa pili kulia), changamoto wanazozipata
kipindi cha masika na kukosa mawasiliano na wenzao wa Wilaya nyingine
jirani.
Mhandisi Mshauri Mr. Sunil Singh
akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani kingo za Boksi Kalvati kubwa lililopo katika barabara za
maingilio ya Daraja la Sibiti, mkoani Singida jana.
Muonekano wa Boksi Kalvati lililopo katika barabara za maingilio zinazoelekea katika Daraja la Sibiti KM 25 mkoani Singida.
Muonekano wa barabara ya maingilio kwa kiwango cha changarawe inayoelekea katika Daraja la Sibiti KM 25 mkoani Singida.
……………………………..
Wananchi wa kata ya Mpambala,
wilaya ya Mkalama mkoani Singida wameiomba Serikali kuhakikisha
inamaliza ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti haraka iwezekanavyo ili
kurahisisha huduma za mawasiliano kati ya wilaya ya hiyo na mikoa jirani
ya Simiyu, Manyara na Mara.
Wananchi hao wamemweleza Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, alipofika
kukagua daraja hilo mkoani humo jana, ambapo pamoja na mambo mengine
wamesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutatatua changamoto za usafiri
hususan katika kipindi cha masika.
“Tunaomba Mheshimiwa Naibu Waziri
utusaidie kukamilisha daraja hili mapema ili tupate huduma muhimu kama
usafiri hasa kipindi cha masika”, amesema mmoja wa wananchi.
Aidha, wananchi hao wameipongeza
Serikali kwa kuendelea na jitahada za ujenzi wa barabara za maingilio
zenye urefu wa KM 25 katika daraja hilo ambapo kwa sasa mradi wote
umefika asilimia 43.9.
Kwa upande wake Naibu Waziri Eng.
Ngonyani ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),
mkoani humo kuhakikisha kuwa wanamsimamia mkandarasi na kuhakikisha
anamaliza ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara hizo kufikia mwezi
Machi mwakani.
Kuhusu deni la mkandarasi huyo
analoidai Serikali, Eng. Ngonyani amesema kuwa watahakikisha wanamlipa
mapema ili kufanikisha mradi kumalizika kwa muda uliopangwa.
“Tutahakikisha tunalipa deni lote
linalodaiwa ili kurahisisha mradi huu kuisha haraka kwa ajili ya
wananchi kuweza kutumia daraja hili pamoja na barabara yake kwa kuwa ni
kiungo muhimu kwao”, amesisitiza Naibu Waziri.
Ametoa rai kwa wananchi wa maeneo
hayo mara tu mradi unapomalizika kuhakikisha wanalinda miundombinu yake
kwani Serikali inatumia gharama kubwa katika utekelezaji wake.
Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS
mkoani humo, Eng. Yohanes Mbegalo, amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwa
atahakikisha mradi huo unaisha kwa wakati ili kuwaondolea wananchi kero
ya usafiri.
Daraja la Sibiti lenye urefu wa
mita 82 linajengwa na mkandarasi China Hanan ambalo linatarajiwa
kukamilika mwezi Machi mwakani na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni
16.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Post a Comment