Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) na Taasisi ya kupigania uhai wa maisha ya wanyama wa mbugani ya
Wildaid Alhamisi Mei 4, mwaka huu kwa pamoja wamesaini makubaliano ya
vita dhidi ya ujangili. Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwakilishi wa taasisi hiyo, Lily Massa.
Akizungumza
kabla ya kusaini makubaliano hayo, Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema
kwamba, “Hii ni sehemu nyingine ya TFF kujihusisha na shughuli za
kijamii licha ya kuwa na majukumu ya kusimamia maendeleo ya mpira wa
miguu katika kukuza na kuendesha mashindano.”
Malinzi
amesema TFF inaendeleza utamaduni wa shughuli mbalimbali za jamii kwani
hata kwa Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Tenga enzi za utawala wake
akiwa kiongozi mkuu wa mpira wa miguu, alifanya hivyo katika kampeni za
kupinga maambukizi mapya ya UKIMWI
“Wengi
mtakumbuka kuwa kulikuwa pia na vita vya kupigania afya za watoto na
kupigania uhai wao pia kampeni za amani ambazo mpira wa miguu umetumika
kuelimisha,” amesema.
Kwa
hatua hii ya sasa, Rais Malinzi amesema kwamba TFF, inaingia
makubaliano hayo na kuiteua timu ya taifa ya vijana Tanzania maarufu
kama Serengeti Boys kusimama kidete kupinga uwindaji haramu wa wanyama
mbugani kwa kuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa
upande wa Mwakilishi wa WildAid, Lily Massa, alishukuru kuingia kwa
makubalino hayo akisema kwamba ndoto zao za kupiga vita uwindaji haramu
na ujangili, itafanikiwa.
“Tunashukuru
kuingia programu hii na ninaamini Mungu atatusaidia,” amesema Massa
ambaye taasisi yake iko karibu kila nchi yenye wanyama wa mbugani.
Katika
hatua nyingine, Rais Malinzi aliitakia kila la kheri Serengeti Boys
ambayo kwa sasa inajiandaa kuingia Gabon kwa ajili ya fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Mei 14, mwaka huu
ambako Serengeti Boys ambayo iko Kundi B itakuwa Libreville - Mji Mkuu
wa Gabon. Timu nyingine za Kundi B ni Mali, Niger na Angola.
Post a Comment