Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), limetoa rambirambi ya Sh 500,000 kwa walengwa walipoteza
watoto katika ajali ya gari iliyoua zaidi ya watu 36, wakiwamo
wanafunzi 33.
Wanafunzi hao 33 wa darasa la
saba, walimu wawili na pamoja na dereva wa gari la shule ya msingi
iitwayo Lucky Vicent ya Arusha, walifariki dunia jana Mei 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa za
kipolisi, vifo hivyo vilivyotokea saa 3 asubuhi baada ya gari walilokuwa
wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu
mkoani Arusha.
Wanafunzi na walimu hao walikuwa
wakitoka shuleni kwao kwenda shule ya Tumaini kwa ajili ya kufanya
mtihani wa ujirani mwema ambako kabla ya kufika basi walilopanda
liliacha njia na kisha kutumbukia korongoni ambako limesababisha vifo
hivyo na majeruhi watatu.
Rambirambi hiyo ya TFF inakwenda
sambamba na salamu za rambirambi zilizotolewa na Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliyeungana na viongozi
mbalimbali akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John
Magufuli katika kuomboleza msiba huo.
Katika salamu zake za rambirambi,
Rais Malinzi amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa
ya vifo hivyo kwani imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa
kulitumikia taifa katika tasnia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa
miguu kama wachezaji, makocha, viongozi hapo baadaye.
“Mtazamo wetu kwa sasa ni
kuendeleza soka la vijana, tena hasa wale walioko mashuleni, hivyo
vijana wale ni sehemu ya kutimiza ndoto za TFF katika mpira wa miguu
hapo baadaye, tunakubali haya yote kwa kuwa ni ya Mwenyezi Mungu ndiye
anayejua siri,” amesema Rais Malinzi.
Salamu za Rais Malinzi zimekwenda
kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva
waliopoteza maisha, akisema: “Huu ni wakati mgumu kwa Wana – Arusha,
wazazi na walezi hawana budi kuwa na subira kwa sasa.”
Amesema kwamba kwa wanafamilia
wote wa mpira wa miguu, “Tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali
pema. Pia wale waliopata majeruhi tunaomba wapone haraka katika ajali
hiyo mbaya.
Ee Mwenyezi Mungu zipumzishe Roho za Marehemu hao, Mahala pema peponi.
………………………………………………………………………………………………
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
Post a Comment