*Asema Serikali yatenga sh. bilioni 412 kwa miradi ya maendeleo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali haina mpango wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala hadi
ikamilishe kuboresha miundombinu kwenye maeneo iliyoyaanzisha.
“Ili kutimiza azma hiyo,
Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi
bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo,
Serikali imetenga shilingi bilioni 16.985 kwa ajili ya kuboresha
miundombinu ya majengo ya ofisi na makazi ya viongozi katika mikoa yote
mipya,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja
ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi
Septemba 5, mwaka huu.
“Katika mgawo huo, mkoa wa
Njombe umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34; mkoa wa Katavi
umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.080; mkoa wa Simiyu umetengewa
jumla ya shilingi bilioni 3.775, mkoa wa Geita umetengewa jumla ya
shilingi bilioni 2.978 na mkoa wa Songwe umetengewa jumla shilingi
bilioni 3.812,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 61.7 kwa ajili
ya ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri 64 ambapo kati ya fedha hizo,
shilingi bilioni 28.7 ni kwa ajili ya kukamilisha majengo ya ofisi
katika Halmashauri 44 na shilingi bilioni 33 ni kwa ajili ya ujenzi wa
makao makuu ya Halmashauri mpya 20.
Sambamba na hatua hizo,
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto
imetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.9
pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri 67.
Waziri Mkuu amesema miongoni
mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuendeleza juhudi za
ugatuaji wa madaraka kwenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja
na kuongeza mgawo wa fedha za ruzuku ya maendeleo inayopelekwa kwenye
vyombo hivyo.
Amesema Serikali inachukua
hatua hizo ili kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini
zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
40480 – DODOMA.
JUMATANO, JULAI 5, 2017
Post a Comment