*Asema ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za mwaka 2002
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema msimamo wa Serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito
kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu umetolewa kwa mujibu wa
Sheria na sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya
wanaharakati.
Waziri Mkuu ametoa ufafanuzi huo
leo (Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano
wa Saba wa Bunge mjini Dodoma.
Amesema msimamo huo wa kisheria
unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao zaidi
badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito.
“Kuwaachisha masomo wanafunzi
waliopata ujauzito ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za mwaka
2002, zinazoruhusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na
makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi, kutumia dawa za
kulevya pamoja na utoro.”
“Lengo hili lina nia ya kuwahimiza
wazazi wawafundishe watoto wao mambo mema ndani ya familia na
wawakataze kushiriki vitendo vya ngono katika umri dhamira ya Serikali
ni kumlinda mtoto wa kike ili apate elimu kwa ajili ya manufaa yake na
Taifa kwa ujumla.”
Waziri Mkuu amesema kila Mtanzania
ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu. Hivyo ni
lazima tuhakikishe mtoto wa kike anapata elimu stahiki na masomo yake
hayakatizwi kwa kupata ujauzito.”
Amesema Serikali imewekeza kwenye
mtoto wa kike, ambapo kifungu Na. 60 (b) cha Sheria ya Elimu Sura ya
353, kinatoa adhabu ya miaka 30 jela kwa yeyote atakayeoa au kumpa
ujauzito mwanafunzi.
Pia, sheria inatoa adhabu ya
kifungo cha miaka mitano jela au faini ya shilingi milioni tano, au
vyote kwa pamoja kwa anayeshiriki kumuozesha mtoto wa shule.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya
kusimamia utekelezaji wa Sheria za nchi zenye lengo la kumlinda mtoto wa
kike. Aidha, nawashauri Waheshimiwa Wabunge, mshirikiane na Halmashauri
zenu kuweka mikakati ya kudhibiti ujauzito kwa watoto wa shule.”
Wahamasisheni wananchi watoe
ushirikiano kwa vyombo vya dola, ili wanaowapa wanafunzi ujauzito au
kuwakatisha masomo ili waozeshwe wapate adhabu stahiki.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
40480 – DODOMA.
JUMATANO, JULAI 05, 2017
Post a Comment