WATANZANIA 1,009 ambao walikuwa nguvukazi ya taifa wamefungwa vifungo vya maisha katika magereza mbalimbali nje ya nchi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa takwimu hizo jana wakati akifunga Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani katika Viwanja vya Nyerere Square mkoani Dodoma. Alisema serikali haitagharamia kuwarudisha nchini wafungwa hao ambao wengi wao ni vijana, lakini kwa taifa linalotaka ujenzi wa uchumi wa viwanda, limepoteza nguvukazi muhimu katika kujenga uchumi wake.
Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya, alisema nchi 21 ambako Watanzania hao wamefungwa ni China watu 265, ambapo kati yao 68 wamehukumiwa kunyongwa. “Nyingine ni Afrika Kusini watu (296), Brazili (121, Kenya (660, Irani (630, India (260), Uturuki (38), Ugiriki (250, Uingereza na Ireland (24) Msumbiji (20), Malasia na Tailand (16), Pakistani (15), Uganda (15), Japan (6), Nepal (4), Comoro (3), Misri (2) na Indonesia, Hispania, Ghana, Nigeria amefungwa mmoja mmoja kila nchi,” alisema.
Alisema tangu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilipoanza Februari mwaka huu hadi mwezi huu, imefanya jitihada kubwa na mabadiliko dhidi ya dawa ya kulevya yameonekana, ambapo ekari 565.75 za mashamba ya bangi katika mikoa mbalimbali nchini zimeteketezwa. “Mikoa inayoongoza ni pamoja na Mara (Tarime na Rolya) ekari 156.75, Morogoro (78), Arusha (68), Kagera (57) na Ruvuma ekari 35.
Aidha, kilo 11,307 za mirungi zimekamatwa na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Mbeya,” alisema. Waziri Mkuu alisema katika kipindi hicho, kilo 1,815 za heroini na kilo 27.58 za kokeni zimekamatwa na katika kipindi hicho hadi kufika Mei mwaka huu, lita 12,890 za kemikali bashirifu zinazotengeneza heroini na kokeni zimekamatwa.
Alisema mamlaka hiyo pia imebaini mbinu mbalimbali za magendo za dawa za kulevya, ikiwemo matumizi ya kemikali bashirifu kwa ajili ya kuzibadilisha na kutengeneza dawa za kulevya. Alisema taifa halitamwacha salama mtu yeyote anayejishughulisha kuanzia wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na hata watumiaji wa dawa za kulevya na kifungo chake ni miaka 30.
“Yeyote anayedhoofisha nguvukazi ya Taifa letu, ana hujumu jitihada za ujenzi wa uchumi wa viwanda na anastahili kushughulikiwa bila huruma,” alisema Waziri Mkuu. “Mamlaka pia imebaini kwamba ziko kemikali ambazo zinatumika kwa ajili ya matumizi halali ya viwandani na kwenye maabara zimeanza kutumika kwa ajili ya uzalishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kisayansi,” alisema.
Waziri Mkuu alimpongeza na kumwagiza Kamishna wa Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyang’a kuhakikisha anawatumia wasanii, wanamuzuki, waigizaji na vikundi vya utamaduni katika kueneza vita dhidi ya dawa za kulevya. Aliwaagiza mawaziri wa Elimu, Sayansi, Ufundi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kuhakikisha zinaundwa klabu za kupambana na dawa za kulevya katika shule mbalimbali nchini kama zilivyoundwa za PCCB na Skauti.
Alimwagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhakikisha huduma za kutoa dawa za kutibu wagonjwa wa dawa za kulevya zinasambazwa katika hospitali za rufaa mikoa na za wilaya. “Tayari zimeanzishwa nyumba za kutibu waathirika wa dawa za kulevya katika hospitali ya Muhimbili, Mwananyamala na Temeke na inajengwa nyingine Dodoma, hivyo ni budi huduma hiyo ya dawa ikasambazwa katika hospitali zote nchini,” alisema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ambayo yalitakiwa kuadhimishwa Juni 26 na kutokana na Sikukuu ya Iddi yakahamishiwa jana ni, ‘Tuwasikilize na kuwashauri vijana na watoto ili kuwapeusha na dawa za kulevya.’
Post a Comment